15 Aprili 2025 - 22:09
Source: Parstoday
Iran: Ufaransa itoe maelezo ya kukamatwa Muirani, mtetezi wa Palestina

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali kitendo cha Ufaransa cha kukataa kutoa maelezo ya kukamatwa Mahdieh Esfandiari, raia wa Iran anayeishi katika mji wa Lyon, kaskazini mwa magharibi mwa Ufaransa, zaidi ya mwezi mmoja baada kutiwa kwake mbaroni na vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya Ulaya.

Habari ya kutoweka kwa Mahdieh Esfandiari, raia wa Iran mwenye umri wa miaka 39 ambaye amekuwa akiishi katika mji wa Lyon tangu 2018, ilitangazwa na familia yake mwezi uliopita wa Machi 2025.

Shirika la habari la Mehr limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, baada ya muda mrefu bila ya kuwepo taarifa zozote kuhusu mwanaharakati huyo, familia ya Esfandiari ilitoa taarifa kwa mamlaka za Iran, na mchakato wa kufuatilia hali ya raia huyo Muirani ukaanza mara moja.

Habari zaidi zinasema kuwa, Esfandiari ni mkalimani na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Lyon, na inaelezwa kwamba alikamatwa mapema Machi mwaka huu kutokana na harakati zake za kuiunga mkono Palestina, na kupinga jinai za Wazayuni katika Ukanda wa Gaza.

Kufuatia juhudi za kidiplomasia za maafisa wa Iran, ilibainika kuwa Esfandiari alikuwa amekamatwa na polisi ya Ufaransa, lakini maelezo ya kesi na mashtaka dhidi yake hayajajulikana.

Hatimaye, gazeti la Kifaransa Le Point liliripoti mnamo Aprili 12 kwamba, mamlaka ya Ufaransa ilivunja ukimya wao wa mwezi mmoja na kutoa habari kuhusu hatima ya raia huyo wa Iran.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mizan, Shahin Hazami, mwandishi wa habari wa kujitegemea na mtetezi wa Palestina, aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii kwamba, Mahdieh Esfandiari alikamatwa baada ya kutuma ujumbe kwenye ukurasa wake wa Telegram, akilaani mauaji ya halaiki yanayoendelea Gaza.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha